Madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka Madaraka kwa Wananchi ambapo chimbuko lake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Sura ya 8, Ibara ya 145 na 146. Upelekeaji wa madaraka kwa wananchi unapitia katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na ndiyo maana Serikali za Mitaa na ushirikishwaji wa Wananchi katika mchakato wa maendeleo vimetambuliwa katika Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati Nchi yetu inapata uhuru wake kulikuwa na majimbo kumi ya Utawala ambayo yaliritihiwa toka utawala wa kikoloni wa Kiingereza mwaka 1966. Rais wa kwanza Hayati Julius Kambarage Nyerere kwa Mamlaka aliyopewa aliunda Mikoa 15 na kuondoa utaratibu wa mgawanyo wa nchi katika Majimbo. Hadi Sasa Nchi yetu ina Mikoa 26, Wilaya 139, Halmashauri 184, Tarafa 570, Kata 3,956, Vijiji 12,319, Vitongoji 64,384 pamoja na Mitaa 4,263. Baada ya uhuru Halmashauri zilikuwa jumla 45 na hadi kufikia mwaka 2009 zilikuwa Halmashauri 129 na zimeendelea kuongezeka hadi kufikia 184 mwaka 2021.
Wakati wa Uhuru hakukuwa na Halmashauri za Majiji na sasa kuna Halmashauri za Majiji 6, kulikuwa na Halmashauri ya Manispaa moja ya Dares Salaam na sasa kuna Halmashauri za Manispaa 20, Halmashauri za Miji zilikuwa 9 na sasa Halmashauri za Miji ni 21 na Halmashauri za Wilaya zilikuwa 10 na sasa zipo Halmashauri za Wilaya 137.
Majukumu ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI
Majukumu ya OR-TAMISEMI yanatekelezwa katika ngazi ya Makao Makuu, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kwa kuzingatia Hati ya Rais ya Mgawanyo wa Majukumu (Presidential Instrument) iliyotolewa na Rais Aprili 2016, majukumu ya OR-TAMISEMI ni pamoja na:-
i) Kuratibu utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Mijini na Vijijini na Upelekaji wa Madaraka kwa Umma (D by D);
ii) Kuratibu huduma mijini kama vile usafirishaji, maji na usafi wa mazingira;
iii) Kusimamia Tume ya Utumishi wa Walimu;
iv) Kuratibu na Kusimamia Tawala za Mikoa ili ziweze kuziwezesha Halmashauri kutekeleza wajibu wake;
v) Kuratibu Usimamizi na Uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari nchini kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM);
vi) Kujenga uwezo wa watumishi wa OR-TAMISEMI ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi; na
vii) Kusimamia utendaji wa Mashirika, Taasisi, Programu na miradi iliyo chini ya OR-TAMISEMI
FOR MORE INFORMATION CLICK HERE OFFICIAL WEBSITE FOR TAMISEMI